MBINU ZA KUSHINDA MASWALI YA USAILI WA KAZI


MBINU ZA KUSHINDA MASWALI YA USAILI WA KAZI
Mwl. Juma
Rununu: +255762957992

Sehemu kubwa ya usaili ni maswali na majibu yanayolenga kupima uwezo wako wa kukabiliana na changamoto halisi za kazi. Ingawa yapo maswali yanayoweza kukupatia wasiwasi wa nia ya mwuulizaji, fahamu kuwa hakuna swali linaulizwa kwa nia mbaya au kwa bahati mbaya.
Kila swali linaloulizwa linalenga kutafuta uthibitisho kuwa wewe ni mtu sahihi wa kazi unayoomba.
Vijana wengi wenye ufaulu mzuri kitaaluma wanaoomba kazi hujikuta pasipokujua wakifanya makosa madogo yanayowagharimu. Kwa kuwa umetumia muda wako kuandika barua, kuandika wasifu wako binafsi wa kazi, wakati mwingine kusafiri kwenda kuhudhuria usaili, ni muhimu kufanya maandalizi yatakayokuongezea nafasi ya kufanikiwa.
Katika makala haya, tutaangazia baadhi ya maswali yanayoulizwa kwenye usaili wa kazi na namna unavyoweza kuyajibu.
1.Mapokezi
Unapokaribisha kwenye usaili, jambo la kwanza ni kuhakikisha kuwa unatengeneza taswira ya mtu anayejitambua, mkomavu na mwenye nidhamu. Salimia jopo linalokupokea kwa tabasamu na salamu ya adabu yenye kuonesha kujiamini. Ikiwa ni lazima kushikana mikono na wanajopo fanya hivyo kwa kujiamini.
Kisha, kuwa mtulivu uelekezwe mahali pa kukaa. Hakuna sababu ya kuwa na papara kukaa mahali hata kama unahisi ndiyo sehemu iliyoandaliwa kwa ajili yako. Unapokaa, kaa mkao unaoashiria mtu mnyenyekevu asiye na makuu.
Mara nyingi kukaa wima ni vizuri na kuambatane na hali inayoonesha kuwa unayo motisha ya kupata kazi unayoomba.
Kunja miguu yako kistaarabu ukikutanisha mikono yako juu ya mapaja kutuma ujumbe wa mtu mtulivu. Egemea mbele badala ya nyuma, watazame wanajopo machoni.
Kwa haraka, wazoee wanajopo kwa kuwaona ni watu wa kawaida lakini wanaostahili heshima.
Unapojibu maswali, epuka kutikisa kichwa. Kukunja nne, kuegemea nyuma au kuweka mikono kwa namna inayoonesha mamlaka ni kutuma ujumbe hasi usiokusudiwa.
2.Utambulisho
Kumbuka kuwa usaili wako ulianza tangu jopo la usaili lilipopokea nyaraka zako. Kwa kiasi fulani, tayari wanayo taswira fulani kukuhusu. Una kazi muhimu ya kuwathibitishia kuwa hayo uliyoyaandika yana ukweli.
Mara nyingi unapokaribishwa kwenye usaili, kiongozi wa jopo la usaili atawatambulisha wenzake. Anapofanya hivyo, ana lengo la kukufanya uwazoee wanajopo, utulie na usiwe na wasiwasi. Shukuru kwa utambulisho wao.
Kiongozi huyo anaweza kukutambulisha wewe kwa jina lako na kukukaribisha maswali. Mara nyingi swali linaloanza ni “Tuambie wewe ni nani? Karibu ujitambulishe
Swali kama hili halihitaji utaje majina yako bali kufahamu muhtasari wako kikazi. Ingawa utakayoyasema yatatokana na uliyoyaandika kwenye wasifu wako wa kazi, mara nyingi hautarajiwi kurudia maelezo hayo.
Jipambanue wasifu wako kikazi na kiutendaji. Jopo linatarajia uwaambie mambo ya msingi unayoyaamini yanaweza kuwasaidia kuelewa mtazamo wako kikazi. Ongelea majukumu ya kikazi uliyowahi kuyafanya ukiyaoanisha na kazi unayoiomba. Anza na kazi ya nyuma zaidi ukimalizia na kazi unayoifanya sasa hivi au ya hivi karibuni zaidi.
3.Ari na uwezo wako wa kazi
Unaweza kuulizwa “Kwanini unafikiri tukuchukue kwa nafasi hii? Kwanini unataka kufanya kazi na sisi?” Watu wengi wanapoulizwa swali hili hufikiri wanachohitaji ni kujilinganisha na wengine kwa majina. Huna sababu ya kuwataja wengine kama namna ya kuonesha unavyofaa zaidi.
Kwa swali kama hilo, kimsingi wanataka kuona kama unaielewa taasisi yao. Thibitisha kuwa umeitafiti taasisi kwa kina na uelewa wa huduma wanazozitoa. Onesha unavyojisikia kuwa sehemu ya malengo mapana ya taasisi yao.
Kadhalika, ni fursa kwako kuonesha namna gani vipaji na ujuzi ulivyonavyo vinaweza kumsaidia mwajiri wako mtarajiwa. Lijibu kwa ujasiri bila kusita. Ukionesha wasiwasi katika majibu yako, wanaokusaili nao watakuwa na wasiwasi na uwezo wako.
Onesha namna gani unafaa kuajiriwa kwa sababu ya uwezo wako.
Katika eneo la ari na uwezo wako wa kazi, unaweza kuulizwa “Unafikiri utaongeza tija gani katika taasisi yetu?”
Hapa ongelea ujuzi na uzoefu wa kazi unaofikiri unaweza kumsaidia mwajiri wako kutatua changamoto alizonazo.
Jitahidi kuonesha namna ujuzi na vipaji ulivyonavyo vinavyoweza kutumika katika maeneo mengine zaidi ya nafasi uliyoomba. Kwa kawaida, mwajiri huvutiwa na mtu anayeweza kutumika katika eneo zaidi ya moja.
Pia unaweza kuulizwa “Unaweza kuniambia mapungufu uliyonayo?” Usiwarahisishie kazi ya kuyaelewa mapungufu yako waziwazi. Waache wao wenyewe wayajue. Badala yake zungumzia mapungufu ambayo mtu akiyatafakari anaona ni tija.
Mfano, “napenda kufanya kazi muda mrefu, napenda kufanya mambo kwa ukamilifu kiasi cha kujikuta sina muda wa kutosha kukamilisha kazi kwa wakati ninaotaka
4.Uzoefu wako huko ulikotoka
Unaweza kuulizwa maswali mengi kuhusu uzoefu wako kazini. Ikiwa kwenye wasifu wako wa kazi ulionesha kuwa uliwahi kufanya kazi mahali na ukaiacha, unaweza kuulizwa swali “Kwanini uliacha kazi yako? Au kwanini unataka kuacha kazi uliyonayo?”  
Hili ni swali gumu. Mwuulizaji analenga kupima uaminifu wako na anataka kujua mambo gani hasa yanakuridhisha kazini. Kimsingi, lengo siyo kujua yalitofanyika huko uliko (kuwa) bali kujua unavyoweza kumfaa. Hutakiwi kuzunguka kwa kutafuta sababu zisizo za ukweli. Jibu kwa urahisi na uwazi lakini ukiwa makini.
5.Matarajio yako kwa mwajiri
Unafikiri tukulipe mshahara kiasi gani?
Hili swali linatafuta kujua vipaumbele vyako uwapo kazini. Ni kweli unatafuta kazi ili upate fedha uboreshe maisha yako. Lakini kuonesha kuwa ari na kujituma kwako kazini kunategemea kiasi cha pesa unacholipwa ni kosa la kiufundi. Kosa hili linaweza kuwa kikwazo cha kupata kazi.
Unatakiwa kuonesha ukomavu kwa kuelewa kuwa taasisi bora kama hiyo unayotaka ikuajiri zina utaratibu rasmi wa kuwalipa wafanyakazi wake. Mtu hulipwa kwa sifa alizonazo. Kwa uelewa huo utapata alama za ziada.
Hata hivyo, pamoja na majibu hayo wapo wasaili wanaweza kukubana uwaambie matarajio yako. Fahamu kuwa kujadili mshahara wa kazi ambayo bado hauna uhakika nayo haiwezi kukusaidia.
Ikiwa utalazimika kutaja tarakimu, inatarajiwa kuwa tayari utakuwa umefanya utafiti wa taasisi hiyo ikiwa ni pamoja na viwango vya mishahara. Taja kiwango ambacho hakitaonesha huna thamani lakini pia usitaje kiwango kitakachoonesha kujikweza kupita kiasi.
6.Uelewa wa mambo na ujuzi wa kazi
Unaweza kuulizwa maswali yanayopima uelewa wako wa kawaida kwa mambo yanayofahamika. Lakini pia unaweza kuulizwa masuala ya moja kwa moja yanayohusiana na kazi unayoomba.
Wakati mwingine, baadhi ya wasaili hutumia mtihani wa kuandika kujaribu kuthibitisha kama kweli una uwezo na ujuzi uliouonesha kwenye wasifu wa kazi.
Maswali yanayoulizwa yanaweza kupima moja kwa moja utaalamu uliousomea darasani au namna unavyoweza kutatua changamoto halisi za kazi. Jiandae ipasavyo kwenye maeneo muhimu.
Kilicho muhimu ni namna unavyoweza kutafsiri nadharia katika mazingira ya kazi.
Kwa mfano, unaomba kazi ya uhasibu msaili mmoja anakuuliza “Chukulia ofisini kwako kumetokea wizi wa fedha. Utachukua hatua gani? Au unaomba kazi inayohusika na utawala “Chukulia kama kiongozi umesikia wafanyakazi wa chini yako wana mpango wa kugoma, utafanyaje?
Hayo ni maswali ya uchokozi. Usitumie muda mrefu kutafuta masuluhisho yasiyokuwepo. Jibu kwa ujasiri kuwa hutarajii kuwa matatizo ya namna hiyo yatajitokeza. Lengo ni kuonesha una uwezo wa kuikinga taasisi yako na changamoto kama hizo.
7.Malengo yako ya baadae
Unajiona ukifanya nini baada ya miaka 10 ijayo? Una malengo gani ndani ya miaka mitano ijayo?
Hapa unahitajika kuonesha ari ya kukua kiujuzi na kiweledi. Ongelea mipango ya kujifunza zaidi kufikia kwenye malengo makubwa yanayoendana na malengo ya mapana ya kitaasisi. Kuzungumzia malengo yasiyoendana na kazi unayoomba kutakupunguzia alama.
Umeomba kazi kwingine?” Wanahitaji kuwa na uhakika na maamuzi yako. Ni kweli inawezekana utakuwa umeomba kazi maeneo mengine. Lakini utaonekana mkomavu ukiweza kuonesha kuwa kazi hii unayosailiwa ndio chaguo la kwanza.
“Utafanya kazi na sisi kwa muda gani?” Hapa wanataka kujua kama wewe ni mpitaji tu au la. Inawezekana kweli unaweza kuwa na mpango wa kufanya kazi kwa muda mfupi na utafute njia nyingine.
Lakini kuonesha wazi kuwa unapita wakati hata kazi hujapata si busara. Onesha ungependa kufanya kazi kwa muda mrefu kadri utakavyohitajika.
“Unaota kufanya kazi gani baadae?” Ukitaja kazi nyingine mbali na hiyo unayoomba, unaleta wasiwasi kuwa hutoridhika na kazi unayoomba.
Ongelea mazingira ya kazi bila kutaja kazi mahususi. Mfano, kazi inayokufanya utumie vipaji vyako na ujuzi ulionao. Kazi inayokufanya ukue kiujuzi na kiuzoefu.
“Uko tayari kuanza kazi lini?” Kama huna kazi ukisema uko tayari kuanza kazi mara moja inaonesha utayari ulionao. Lakini kama unabadilisha kazi kuonesha utahitaji muda mfupi wa kukamilisha taratibu za kukabidhi majukumu uliyonayo na kuaga itakupatia alama.
8.Fursa ya kuuliza swali
Kwa kawaida, baada ya kuulizwa maswali mengi, kikao cha usaili kitahitimishwa kwa kukukaribisha kuuliza swali. Kama tulivyosema, kila swali lina maana kwenye usaili.
Unapoulizwa “Je, una swali ungependa kuuliza?” Lengo ni kutaka kujua ulivyo na ari ya kufanya kazi na taasisi hiyo.
Usipouliza swali lolote, maana yake ama huna uelewa wa mambo mengi au huna ari ya kutosha. Uliza swali kuhusu taasisi hiyo. Waulize wanatarajia nini kwa mtu atakayepata kazi hiyo.
Kadhalika, waweza kuulizia mambo yanayohusiana na fursa wanazoweza kutoa kukuza ujuzi wako kama mfanyakazi wao.
Epuka kuuliza maswali ya kimaslahi. Kuuliza “Mnanilipa bei gani?” ni kuonesha huna mtazamo mpana na kazi. Unaweza hata usijibiwe au ukajibiwa jibu litakalokunyong’onyeza.

Ahsante.  
 
  
  

No comments

Theme images by jangeltun. Powered by Blogger.