IKIRARI NA HAKIMILIKI
Mimi JUMA PETER ninathibitisha kwamba
mashairi haya ni yangu, na kwamba sijanakili wala kulahamu kwa namna yoyote
ile, na hayajawahi kuwasilishwa wala hayatawasilishwa katika chuo kikuu kingine
chochote kwa ajili ya kukidhi matakwa ya kitaaluma ya kozi za ubunifu na utunzi
wa kazi bunilizi za kifasihi.
Haki zote zimehifadhiwa. Hairuhusiwi
kuzalisha, kuiga, kunakili, kutafsiri, kupiga chapa kwa namna yoyote iwayo wala
kusambaza sehemu yoyote ya mashairi haya kwa namna yoyote ile bila kibali cha maandishi
kutoka kwa mwandishi.
ANUANI YA MTUNZI:
Mwl. Juma Peter
S.L.P 1226
Moshi-Tanzania
Rununu: +255762957992
Barua pepe: jumapeter399@gmail.com
ISBN: 978-9976-5318-0-7
Sehemu ya matini tepe hii ya mashairi yanapatikana
katika kitabu change cha mashairi kiitwacho JICHO LA KURUNZI kimechapwa na:
Beanna
Printing Solutions
Morogoro Tanzania
+255766770422, +255713360853
SHUKURANI
Namshukuru Mungu wa Mbinguni aliyenipatia ujasiri na mawazo ya kutunga
mashairi jina la Mwenyezi Mungu muweza wa yote lihimidiwe.
Nawashukuru walimu wangu wote kwa kunifundisha katika ngazi tofauti
tofauti za Elimu na taaluma kuanzia Elimu ya Msingi hadi Chuo Kikuu. Napenda kuwashukuru
wahadhiri wangu wa kozi za Fasihi na Isimu wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Mwenge
kilichopo Moshi-Kilimanjaro kwa moyo wao wa dhati kunielekeza mambo mbalimbali
ya kitaaluma ambao ni Rick Ngowi, Musa Sultani, Deogratius F. Mkawe, Sr. Rehema
Mkundiwe na Furaha J. Masatu. Sambamba na hilo nawashukuru sana wahadhiri wangu
wa kozi ya KIS 206 Uandishi wa Kubuni I na KIS 305 Uandishi wa Kubuni II;
Mwalimu Eric Ndumbaro na Mwalimu Furaha J. Masatu ambaye nimeshamtaja awali kwa
ushauri wao mzuri kuhariri mashairi yangu hakika Mungu awalipe muda wenu mlioutumia
na msonge mbele zaidi.
Niwashukuru kwa dhati wazazi wangu niwapendao Peter Emanuel na Beatrice
J. Hamisi, dada zangu Neema Peter na Stela Peter, Kaka zangu Stephano
Peter, Yusuph Peter na Daniel Peter kwa kunilea na kunisaidia kwa upendo wao
usio kifani hata kuniwezesha kushiriki kutunga mashairi.
Pia shukrani zangu za dhati ziwaendee wahariri na wasomaji prufu wa
mashairi yangu walioshirikiana nami katika kukamilisha kazi hii kwa kunitia
moyo si rahisi kuwataja kwa majina yao yote lakini wachache ni hawa; Erick
Ndumbaro, Furaha J. Masatu, Masanja Jilala, Eston Salvatory, Faki Sheha na Hijiraimu.
Nitakuwa mchoyo wa fadhila nisipowashukuru marafiki na wanafunzi wenzangu
wa mwaka wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki Mwenge kwa kozi zote, siwezi kuwataja kwa
majina yao yote lakini wachache wao ni pamoja na Masanja Jilala, Damas Meshack,
Zengo Michael, Yohana Philemon na Shelly Renatus kwa maoni yao mazuri Mungu awabariki.
IKISIRI
Mashairi
ya mwalimu Juma ni miongoni mwa zao katika kozi za Uandishi wa kazi
bunilizi za fasihi. Mashairi yanaeleweka
kwa wasomaji kwani yametumia lugha inayoeleweka na iliyopikwa vizuri yenye
misemo, taswira, matumizi ya picha, tamathali za semi, na mbinu nyingine za
kisanaa hivyo inaleta burudani kwa msomaji pindi asomapo.
Mashairi
haya yamepikwa vizuri kwa kuitalii miundo mbalimbali ambayo huongoza utunzi wa
mashairi kwa kurejelea kanuni za umapokeo kwa kiasi kikubwa kwa kuyasawiri
mambo mbalimbali ambayo yako katika jamii hasa kwa kuyafichua na kuielimisha
jamii ili iweze kuyaepuka.
Vilevile
mashairi haya yanatoa maonyo kadha wa kadha ambayo jamii haina budi kuyapokea
ili iweze kuendana na mazingira halisi ya watanzania kwa kuwa na mienendo
mizuri, kufanya kazi na kuepuka wimbi la utegemezi pindi watu wanapotafuta
maisha kwa lengo la maendeleo binafsi na jamii kwa ujumla wake. Pia mashairi ya
mwalimu Juma yanatoa mwanga kwa jamii namna ya kuishi na kuzikabili
changamoto mbalimbali zilizopo katika jamii na zinazoyakumba makundi mbalimbali
ya watu hasa vijana ambao ndio Taifa la kesho.
Na
Mwl Juma.
Visafi
vyatamanika, sitiri yake vichafu
Vichafu visopendeka, vile vya kichefuchefu
Chefu yule wake taka, chanzo cha uharibifu
Kiliwacho
ni uchafu, sharti yake unawe.
Vyatawanya kila zoni, kumbe navyo ni uchafu
Kunyaka kwazo pupani, mnyako uso faafu
Bila haya uzunguni, ukahamia kwa tifu
Kiliwacho
ni uchafu, sharti yake unawe.
Chakula nacho uchafu, sharti yake unawe
Wenye vilemba mfu, vilowabebea mawe
Nje makaburi faafu, ndani yajaa kiwewe
Kisafi
nacho kichafu, kama fumo mwenda chini.
Fikrani vyanijia, vile vya kichefuchefu
Nani alopulizia, dawa mjifanye wafu
Zao taka walofia, kufanya urembo mfu
Kisafi
nacho kichafu, sharti yake unawe.
Ubongo tujivunie, kama tulo na ubongo
Vya asili jivunie, kwa nguvu kama wabongo
Uzalendo tuenzie, kama tusokunywa gongo
Kichafu
kiwe kichafu, tupende uzuri wetu.
CHURA
Na Mwl Juma.
Chura
kuishi shirika, ndiyo yao tamaduni
Si
shaka yafahamika, ndivyo tangia zamani
Wa
jina la kusifika, ndiye chura wa majini
Ukweli wajulikana, kwa miongo
na miongo.
Kwa
mie yanonijia, katu yaso kawaida
Kuwaza
na kuwazua, kiumbe aso na shida
Kwenye
mito kuzagaa, maji ni yake faida
Yote haya kawaida, kwa wa jana
na wa leo.
Wakaishi
kwa furaha, majini vyakula tele
Amani
bila karaha, mwendo wa vigelegele
Umoja
kwao silaha, katu pasina kelele
Hii yao kawaida, vyura wakazi
wenyeji.
Ghafla
chura kajawa, yake mambo fikrani
Kutaka
kuhama bwawa, kubadili maskani
Hataki
kushauriwa, chura yule wa majini
Kweli chura kaamua, atengane na
wenzake.
Tarehe
ikawadia, yake chura kufungasha
Ugenini
kuhamia, nchi kavu karibisha
Taratibu
mazoea, mitindo ya kupotosha
Na shughuli kuzifanya, tena
nasema haramu.
Si
ndoto chura mgeni, ukwasi kujivutia
Magari
kwake nyumbani, ngome kuyazungushia
Masikini
asilani, dharau kwao kutoa
Hakujua ni masika, kiangazi
kinakuja.
Ukame
ukawadia, nchi kavu yote jangwa
Na
jua likasogea, chura mali zikalengwa
Ardhi
kujichimbia, mvua kwake ni lengwa
Ardhi ikachemka, kama moto
uwakao.
Kufumba
na kufumbua, chura yu jasho mwilini
Tena
akishangilia, kwa makofi ardhini
Akilini
akijua, mvua i vuruguni
Mwanzo ukawa kwa chura,
kuumbuka ugenini.
NGULI WA VICHEKO
Na Mwl Juma.
Kumezuka
mashindano, yasobagua jinsia
Yalo
pa msongamano, yeyote kutamania
Liso
shindano la ngano, vicheko kushindania
Huyu yule achekaye, wa mwisho
hucheka sana.
Vikawekwa
vichochezi, nia cheko kutokea
Kwa
stori za makuzi, tena chuku kuwekea
Cheko
zikawapa kazi, haya zikawakimbia
Huyu yule achekaye, wa mwisho
hucheka sana.
Pasi
kujali u nani, kwako kucheka kuloje
Chekozo
zahusu nini, kwakezo zimekomaje
Nacho
cha taimu gani, mimosao ‘metekaje
Huyu yule achekaye, wa mwisho
hucheka sana.
Washindani
mso macho, kuwa kodo mchekapo
Kwani
kipo kikulacho, epuka kucheka papo
Hata
kiso chakulacho, mwanzo usicheke hapo
Huyu yule achekaye, wa mwisho
hucheka sana.
Wa
mwisho hucheka sana, epuka kucheka mwazo
Wache
wachochee mwana, usijegeuka kenzo
Cheko
mwanzo huchoshana, mithili betri chenzo
Huyu yule achekaye, wa mwisho
hucheka sana.
BLUUTUTHI
Na Mwl Juma.
Hodi
hodi simu janja, mliopo madukani
Ndiyo
simu wa viganja, vidole mtelezoni
Wasofichwa
kama ganja, wenye hofu ya mbaroni
Simu janja ni ujanja, bluututhi
ya nini?
Fikrani
kunijia, pawani bluututhi
Kuwaza
na kuwazua, utisho uso hadithi
Kunusa
chipsi njaa, pasi hati ya urithi
Simu janja ni ujanja, bluututhi
ya nini?
Wacha
wako uchokozi, kumezea ungo mate
Imekuwa
yako kazi, wa mbalini uwanate
Yako
kodo waziwazi, mwenye pete yako tete
Simu janja ni ujanja, bluututhi
ya nini?
Kufumba
na kufumbua, mapono yakawa visa
Dumuzi
ukaletea, vinyonyi kwa samakisa
Pawani
zote kufia, mithili yake mimosa
Simu janja ni ujanja, bluututhi
ya nini?
Langu
moya nakuuma, sikioni ung’amue
Bluututhi
ya kiyama, vipanya jiepushie
Njia
kuu iwe mama, hapa huku zifukie
Simu janja ni ujanja, bluututhi
ya nini?
KIJIBA CHA MWITU
Na Mwl Juma.
Binti
mwali uso mwali, kwa sie nini wataka
Takozo
zisopo tuli, shebeduzi zisonyaka
Mtimako
kawa tuli, mahaba huba kutaka
Neema uso na wema, ulo kijiba
cha mwitu.
Kinandacho
ukateka, mara hisia kudata
Ya
kisomoni kutaka, bila furushi la data
Wodi
ya jiba kutaka, darasa lenye utata
Neema uso na wema, ulo kijiba
cha mwitu.
Sautiyo
yawa pingu, kuteka kila hadhira
Takozo
milio bangu, walo sumu kukuchora
Kuvimba
yao marungu, kupiga alowachora
Neema uso na wema, ulo kijiba
cha mwitu.
Punde
rungu lipokuja, yake kutimiza kazi
Kajifanya
kuyachuja, eti sawa na mzazi
Bohari
likayafuja, mbio zilo waziwazi
Neema uso na wema, ulo kijiba
cha mwitu.
Kila
rungu lipopata, wake mtima kusuza
Lako
Ini kujikata, kwa wivu ulo na kiza
Marungu
yalokufata, kwayo chuki kuikuza
Neema uso na wema, ulo kijiba
cha mwitu.
Langu
wazo chukueni, ulompenda mwambiye
Wali
ukimya wacheni, zenu haya zikimbiye
Bwangai
chuki wacheni, adili wema nduguye
Neema uso na wema, ulo kijiba cha
mwitu.
NANI ATOKE!
Na Mwl Juma.
Wetu
yehova twaomba, mtukufu yako sifa
Wako
viumbe twaimba, sikie nyimbo za sifa
Za
mseto na marimba, kama enzi za kayafa
Lugha ndiyo yetu nyenzo, zetu
haja kutimiza.
Punde mola kuifanya, yetu sayari dunia
Kiumbe
mtu na panya, na wengine kutokea
Kama
mchanga wa sanya, ubaguzi kuzukia
Jipu baya hili bovu, kama fumo
mwenda chini.
La
fikirisha akili, si kwa yule wala huyu
Kijeba
mtu mbigili, uvae pete ya mbuyu
Mawazo
yaso adili, kila uchao mabuyu
Nomino yake tatizo, ubwangai
yako kazi.
Makundi
yaso shirika, yakaundwa ya kisomo
Dhaifu
kusaidika, kupata yao kipimo
Nakiri
pasina shaka, kisomo kiso kikomo
Kurushiana arafa, za kutegua
mitego.
Nawaza
na kuwazua, washirika chapuchapu
Pasi
shaka jiungia, ya mitandao wasapu
Idadi
kujipangia, kuhofia kwa majipu
Mawazoni kunijia, wasapu ya
kijamii.
Bila
hili wala lile, tangazo wasapu hilo
Alozidi
sio yule, kibwangai jasho hilo
Kigugumia
si kwele,asipingane na hilo
Kwa huzuni kutamka, basi wa
mwisho atoke.
Punde
sakata epapu, kumvaa adimini
Kwa
kuondoa wasapu, jina pasipo idhini
Kwani
kibwangai jipu, kujisafisha ummani
Hili jipu
baya bovu, sharti litumbuliwe.
MAKALIO
Na Mwl Juma.
Yatutekenya hisia, Kwa ukubwa makalio
Wapenzicho kusifia, kuvuta makumbatio
Mwili
ganzi kuzimia, yatikisapo milio
Yawe madogo makubwa, huyu yule
kujivuna.
Dereva
kichwa kuhimwa, mwendo kuingiza gia
Kasi
mshale kusomwa, juu ya asilimia
Katu
taa kutozimwa, hapa huku jivunia
Yawe madogo makubwa, huyu yule
kujivuna.
Mvua
kuyasitawisha, kiburi kukuzidiya
Midomo
kuitepesha, jiona wakamiliya
Bia
zako kuzichosha, kuusambaza umbeya
Yawe madogo makubwa, huyu yule
kujivuna.
Makubwa
yamegeuka, asali kuwa shubiri
Macho
nayo kukodoka, ukame kukushamiri
Madogo
kutamanika, katu bohari kukiri
Yawe madogo makubwa, huyu yule
kujivuna.
Wengio wamegundua, kweli za
yako maisha
Ubwangai twaujua, usiku
wajionesha
Madume kuwachekea, garini
kujipitisha
Yawe madogo makubwa, huyu yule kujivuna.
Kila dume lakubeba, maradhi jichukulia
Na UKIMWI kuubeba, sababu yako
tamaa
Gonjwa lisilo na tiba, nguvu
kazi yapotea
Yawe madogo makubwa, huyu yule kujivuna.
Zangu ndugu sikieni, sidate na
makalio
Langu somo sikieni, elimu kwenu
kioo
Nzuri tabia enzini, kwenu iwe
kumbatio
Yawe madogo
makubwa, huyu yule kujivuna.
ANUANI YANGU
Na Mwl Juma.
Nina
habari muhimu, kwenuni zangu maisha
Sina
budi kusalimu, kwa heshima za kutosha
Kwa
saluti za adhimu, pasina kumng’unyisha
Heshima kwao wazazi, kunilea
tangu kinda.
Kumbukumbu
zanijia, tanguzo kinda maskani
Utimamu
kunijia, kablapo baleheni
Tisa
miaka najua, kwa eskoti shuleni
Makala yangu nomino, maskani
julikana.
Nyisanzi
tanguzo shule, la kwanza langu darasa
Mwaka
sufuri mbilile, pale kati ziso tasa
Alfani
mbili ile, omegani tatu hasa
Yangu kodo waziwazi, vidudu
kuvifagia.
Chato
kwa Magu nikawa, vidudu nikasomea
Pale
la tano likawa, darasa nilosomea
Chenjile
shule ikawa, Kahama nikahamia
Kakola shule ikawa, langu saba
kutimia.
Mwaka
ishirini kumi, changu kwanza kidatoni
Miaka
minne mumi, nikatimiza foleni
Foleni
nilopo mimi, iso mithili ya buni
Ufaulu kunijia, tunu faraja ya
wengi.
Julai
yangu safari, changu cha tano kusoma
Kwa
furaha bila shari, kisomo pasina homa
Langu
bohari kukiri, ulofata ukakoma
Maharageyo kwaheri, mwendo wa
vigelegele.
Papu
neti ikatema, naona matini tepe
Yangu
machoni kusoma, mwendo wa barua pepe
Si
kama yule wa homa, ilomkata mapepe
Pundeni hodi getini, Makala
naye Mwekau.
Zangu
jama sikieni, wa Mwekau furahini
Shika
yako kisomoni, mithili yake kunguni
Imarisha
tamrini, ya nduguze mtihani
Mshike sana elimu, usimwache
atoroke.
WAIFII
Na Mwl Juma.
Kumezuka dijitali, tali mithili ya wali
Isozimika
kwa chali, moto ule wa ugali
Muwako
kama adili, si nduguze wa adili
Hadhi yake simu janja, waifii
mdatoni.
Waifii
yenye kasi, pasi shaka yake jeti
Jeti
iendayo kasi, katu pasina kubeti
Kubeti
kwa wasiwasi, simu hofu ya umati
Hadhi yake simu janja, waifii
mdatoni.
Mwenye
pawa ya ajabu, nani mwenye uthubutu
Uthubutu
wa jawabu, jawabu lenye ukutu
Kutu
pasina kutubu, waifii wacha butu
Hadhi yake simu janja, waifii
mdatoni.
Waifii
mdatoni, kudata simu za hadhi
Kusaliti
wa tochini, pasi shaka wenye hadhi
Konekiti
wa nguvuni, kama mito ya ardhi
Hadhi yake simu janja, waifii
mdatoni.
Langu
moya nakuwasa, zoea chako kikavu
Kavu
mithili ya kasa, kasa mgeni wa kuvu
Yako
manyoya usasa, yauwayo kama kuvu
Hadhi yake simu janja, waifii
mdatoni.
GEREZA BUBU
Na Mwl Juma.
Kumetokea
malezi, malezi yaso baraka
Si
ya wawili wazazi, kwa bayana natamka
Watu
wenye zao kazi, watoto kuajirika
Mazuri mengi majumba, siri
nyingi kufichika.
Wenye
vyao kusafiri, sehemu za mashambani
Jitwalia
bila shari, mabinti kuwapa fani
Cha
ajabu la hatari, si ndoto usingizini
Kazi wasotarajia, pasi ombi
kuzifanya.
Si
kazi ya masihala, kwa bayana naeleza
Hekalu
lake mhola, kwa shuruti kuliuza
Kwa
madhumuni mihela, mwajiri kujitanuza
Mazuri mengi majumba, siri
nyingi kufichika.
Kwa
nyumba wake ulinzi, kama nyuki mzingani
Hujaona
tangu enzi, ndoto kupita getini
Katu
langoni mlinzi, pia hutomrubuni
Mazuri mengi majumba, siri
nyingi kufichika.
Mateso
kuendelea, mabinti haki kukosa
Nani
wa kuwaokoa, jamani mso na kosa
Jamii
yote dunia, fichua hii ni kansa
Gamba la kasa mkubwa, yule
mwenye siri nyingi.
URAIA NCHI MBILI
Na Mwl Juma.
Wetu Mola mtukufu,
Ulo na wema kunjufu
Pendo liso na turufu
Hapana wa
mithiliyo.
Kwako viumbe vikawa
Majini napo vikawa
Nchi na anga vikawa
kwa matamko
vikawa.
Kupendelea ikawa
kufanya mtu ikawa
Dongo kufanya ikawa
Kuyafinyanga tukawa.
Vyote ulotamkia,
Tena pasi kujalia
Maelfu kwa mamia
Majini na nchi pia.
Viliwavyo kagawia
Vya asili nakazia
Viso sumu nasemea
Bayana natamkia.
Tamko kusainia
Kwa peni isobungua
Andishi lilo wasia
Mtimani kuwekea.
Mwanzo mlo wa adili
Viko wapi vya asili?
Fahiwani nakubali
Ugenini mwakubali.
Maradhi mwajibebesha
Kisukari kwa presha
Vya fati kujikuzisha
Visa mtindo maisha.
PETE
ISOVULIKA
Na Mwl Juma.
Pete kito cha thamani, amani kwake moyoni
Isotoka
kidoleni, ndiyo pete ya moyoni
Mtima
mtulizoni, kwa pete iso rangini
Amani kwake mtimani, pete kito
cha thamani.
Jama
pete isotoka, nini siri ya kudumu?
Isopenda
kupotoka, kama funiko la dumu
Ikadumu
kuzunguka, mithili ya gurudumu
Pete kito cha thamani, amani
kwake mtimani.
Wakariri
chako chanda, usivaliwe kwingine
Majirani
walopinda, kachoma kama senene
Zao
shingo zikakonda, kutaka zuri unene
Pete kito cha thamani,
hakivaliwi kwingine.
Jirani
wakumezea, zao kodo kukodoka
Kwa
hila kuichukua, wakijua itavika
Pete
ikawazibia, lake tundu kuvalika
Pete kito cha thamani,
hakivaliwi kwingine.
Na Mwl Juma.
Zamanizo za matenga, yafumwayo kwazo nyasi
Nyasi kusitiri menga, menga isoleta wasi
Wasi kwakezo mkinga, jama mbeba fenesi
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Miongo ‘tano mepita, matenga yayo meona
Meona anko lapwita, matunduye yasobana
Bana makubwa kupita, chini madogo bayana
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Lake anko labagua, mafenesi ilobeba
Beba kubwaga chunjua, kama ndizi za muleba
Leba ya mama kulia, mithili kwayo maleba
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Bila woga kupanua, kwakezo kupe matundu
Tundu lililowaboa, kupita pasina gundu
Gundu liso kubebea, kasoro za seli mundu
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Tengani matundu lango, vigezo umepanua
Panua yake mipango, hofu kufuga kwelea
Kwelea aso maringo, safi hewa kuiua
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Matundu yamechukiwa, si kupe wala kunguni
Nguni hata mbu mekuwa, kukosa keki tengani
Ngani kuwatoa yawa, bila huruma ummani
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Wengio waso tengani, walo sifa za tengani
Ngani kuvuta kwa kani, pasi hongo ya kihuni
Huni mbio za mwituni, furaha mtelezoni
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Tenga la anko mependa, anko pasi shaka Magu
Magu mtu aso kinda, afagiaye magugu
Gugu sugu la kupinda, mithili yakeyo sugu
Wetu anko tafrani, lakelo tenga ni kwele.
Dunia
si kama shuka, unayoweza kushika
Sijifanye
mhusika, wa dunia Kama shuka
Mabaya
kuyatamka, na kwa watu kusikika
Hasidi
ubadilike, jaribu kuelimika.
Takonda
kwa roho mbaya, na dawa katu haipo
Chuki
ni safura piya, tena bila ya malipo
Hakuna
wakukulipiya, popote pale ulipo
Yakupasa
zingatia, sote ni waja wa mungu.
NYAMA YA ULIMI
Na Mwl Juma.
Wengi wetu mesikia, wasomi wa vitabuni
Vyake dini nakazia, maandiko ya mwangani
Madhambi kuyakemea, kwa shuruti si utani
Yote haya twayajua, hata wale wa mizimu.
Pasi chenga yaeleza, bayana kufafanua
Kiungo chenye kumeza, ulimi sote twajua
Kama njiti ya kumeza, misitu ya Tanzania
Ulimi kitu hatari, pasina pingu huuwa.
Kiumbe usiyejua, kuchagua la kunena
Nani amekugawia, ganja isiwe banana
Ushauri kukataa, nakueleza bayana
Acha wako unafiki, ukinyonga kuuvua.
Ndogo chembe hatari, si wakomavu wadogo
Katu bila tahadhari, huchoma hata magogo
Daktari wake siri, ukimya pasina pigo
Sina budi kuunena, ukweli shubiri chungu.
Kuuweka wako pingu, ulimi bila dhamana
Kuuondoa uchungu, ule wa maji ya kana
Wenye kufunika mbingu, migogoro kutokana
Wekea pingu ulimi, misitu isitoweke.
UTOMVU WA PAPAI
Na Mwl Juma.
Ndugu zangu sikieni, wasia ulo upendo
Pasi shaka pokeeni, wasiani uso fundo
Wabichi wakomaani, meupe maji mrindo
Jama
maji tiba sumu, utomvuni mwa papai.
Kwake rangini kufana, mithili yake maziwa
Majini kusonatana, si mgando maziwa
Utomvu maji kulina, yake meupe ni dawa
Jama
maji tiba sumu, utomvuni mwa papai.
Utomvuni mwa papai, usokauka shipani
Mithili yake mayai, mwa kaka mzungukoni
Tena yake maji ai, faranga kwake nyumbani
Jama
maji tiba sumu, utomvuni mwa papai.
Watumiwa kama dawa, ngozini kuitepesha
Vijidudu kuviuwa, sirosisi kuifisha
Viharusi wafukiwa, makaburi ya kutisha
Jama
maji tiba sumu, utomvuni mwa papai.
Utomvuni tiba sumu, pasi huruma huvuma
Mithili yake kisumu, dawa vitambi vya zama
Kufa kwake kuvu sumu, mithili yake ukoma
Jama
maji tiba sumu, utomvuni mwa papai.
Wangu wasia utomvu, ule wa maji meupe
Upakwao kwa mashavu, kwa mapozi ya utepe
Wabichi kwa wakomavu, mwe makini na meupe
Jama
maji tiba sumu, utomvuni mwa papai.
TAARIFA MUHIMU KUHUSU MWANDISHI
Juma Peter alizaliwa tarehe 20 mwezi Desemba mwaka wa
1993 katika Wilaya ya Iramba Mkoani Singida na baadaye kupata Elimu katika
shule ya Msingi Nyisanzi iliyopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita kuanzia mwaka
2003-2007, ndipo alihamia Shule ya Msingi Kakola “A” iliyopo Wilaya ya Kahama
Mkoani Shinyanga 2007-2009. Baadaye alijiunga na Elimu ya Sekondari katika
shule ya Sekondari Bulyanhulu iliyopo wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga na
kutunukiwa Certificate
of Secondary Education Examination (CSEE) 2010-2013. Mwalimu Juma Peter
alifaulu mtihani ya kidato cha Nne na kufanikiwa kuendelea na masomo ya kidato
cha Tano na Sita katika shule ya Sekondari Itigi iliyopo Wilaya ya Manyoni
mkoani Singida katika Mchepuo wa HGK na kutunukiwa cheti cha kuhitimu kidato
cha Sita yaani Advanced
Certificate of Secondary Education Examination (ACSEE) 2014-2016. Badaye
alifaulu mitihani yake ya kidato cha Sita na mwezi Oktoba 2016 alifanikiwa
kuchaguliwa kujiunga na Elimu ya Chuo Kikuu katika Chuo Kikuu Cha Kikatoliki
Mwenge kilichopo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro kusomea Shahada ya Kwanza
ya Elimu Sanaa yaani Bachelor of Education in Arts (Jiografia na Kiswahili).
No comments