MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOJIANDAA NA USAILI (INTERVIEW) YA KAZI
MAMBO YA
KUZINGATIA UNAPOJIANDAA NA USAILI (INTERVIEW) YA KAZI
Mwl. Juma,
Baruapepe: jumapeter399@gmail.com
Rununu: +255762957992
Kuitwa kwenye usaili wa kazi ni
hatua ya mwisho kuelekea kupata ajira uipendayo. Mara nyingi kazi inapotangazwa
waombaji wa kazi hiyo huwa ni wengi. Baada ya kupokea maombi ya kazi, shughuli
inayofuata ni kufanya uchambuzi wa kuwatambua waombaji wanaokaribia vigezo
vinavyohitajika. Matokeo ya uchambuzi ni kupatikana kwa orodha ya watu wachache
wanaoitwa kwa hatua ya mwisho ya uombaji wa kazi.
Kwa kuwa si watu wengi hufikia
hatua hii, unapopata taarifa rasmi kuwa umeitwa kwenye usaili wa kazi
uliyoiomba, ni jambo la kujivunia. Kuweza kushindana na kundi la watu wengi
waliohitaji kazi hiyo na hawakuitwa si jambo dogo.
Hata hivyo, ni vizuri kutambua
kuwa usaili wa kazi sio kupata kazi. Wapo watu waliowahi kuitwa kwenye usaili
mara nyingi lakini hawakupata kazi. Makala haya yanakupatia dondoo chache za
kukusaidia kufanya usaili wenye mafanikio. Lengo la makala haya si kujadili
makosa wanayofanya watu kwenye usaili.
Yafuatayo ni mambo halisi ya
kukuwezesha kushinda usaili na kupata kazi.
1.Elewa malengo ya usaili
Huwezi kujiandaa vizuri kwa ajili
ya usaili bila kuelewa malengo ya usaili. Kwa kawaida, usaili ni mahojiano ya
kati ya mwombaji wa kazi na mwajiri kwa lengo la kutathmini uwezo wa kikazi
alionao mwombaji.
Mahojiano haya aghalabu hufanyika
kwa mazungumzo au maandishi katika chumba au eneo lolote linaloteuliwa na
mwajiri kwa kazi hiyo.
Hata hivyo, si lazima mwajiri
awepo kwenye usaili. Wakati mwingine mwajiri hukaimu mamlaka yake kwa watu
anaowaamini kwa kazi hiyo. Jopo hilo hufanya kazi ya kukusanya taarifa
zinazotumika kufanya maamuzi ya ikiwa mwombaji wa kazi anaweza kuajiriwa au la.
Kwa muktadha huu, kinachoamuliwa na jopo hilo halali kinawakilisha matakwa
halisi ya mwajiri.
Jambo la msingi kuzingatia ni
kuwa unapokwenda kwenye usaili wa kazi, una wajibu wa kuthibitisha kuwa unafaa
kwa nafasi ya kazi unayoiomba. Hilo litawezekana ikiwa utaonesha namna uwezo
wako, maarifa yako na ujuzi ulionao yanavyowazidi watu wengine wanaoshindana
kupata nafasi hiyo unayoiomba.
2.Fanya utafiti wa taasisi
Maandalizi yanaanza kwa kufanya
utafiti wa taasisi unayotarajia ikupatie kazi. Uelewa wa taasisi ni muhimu kwa
sababu maswali mengi utakayokabiliana nayo siku ya usaili, kwa kiasi kikubwa
yanategemea namna unavyoielewa taasisi unayotaka ikuajiri.
Katika kufanya utafiti, unahitaji
kuelewa historia ya taasisi, dira na malengo yake, mfumo wa utendaji wake,
uongozi wake, walengwa katika huduma zake na mambo kama hayo. Uelewa wa kina
maeneo hayo utakusaidia kujibu kwa ufasaha maswali yanayoweza kujitokeza siku
ya usaili.
Ili uweze kufanya utafiti,
unahitaji kufuatilia tovuti ya taasisi hiyo, kurasa za taasisi katika mitandao
ya kijamii na machapisho mbalimbali yanayopatikana mtandaoni.
Kadhalika, unaweza kuwasiliana na
watu wanaoifahamu taasisi husika na kujaribu kupata taarifa zitakazokusaidia.
3.Jiandae kisaikolojia
Sambamba na kufanya utafiti wa
taasisi husuka, unahitaji kuiandaa akili yako kwa ajili ya siku ya usaili.
Amini upo uwezekano mkubwa wa kupata kazi uliyoitiwa. Unapokuwa na mawazo
chanya ni rahisi kujenga hali ya kujiamini itakayokusaidia kufanya vizuri zaidi
kwenye usaili.
Ni makosa kwenda kwenye usaili
hali ukiamini hutopata kazi. Hisia kuwa unatimiza mradi tu zitakuondolea nguvu
ya kufanya vizuri.
Hata kama ni kweli mara nyingi
umeitwa kwenye usaili wa kazi na hukufanikiwa, amini kuwa safari hii utapata
kazi. Imani inajenga kujiamini, kujiamini kunajenga ujasiri.
Kama una wasiwasi na kujiamini
kwako, tafuta watu wenye maneno ya kuinua moyo wakusaidie. Soma maandiko
yanayokuinua moyo. Kwa kusikia na kusoma maneno yanayokujenga utaimarika
kisaikolojia na kuwa jasiri zaidi.
Sambamba na hilo, epuka kuongea
na watu wanaokukatisha tamaa wanaokuonesha kuwa hutopata kazi. Ukijiruhusu
kukutana na watu wa namna hii, utaishia kuvunjika moyo na utashindwa kufanya
vizuri.
4.Hakiki muda na mahali pa usaili
Kosa kubwa unaloweza kulifanya
siku ya usaili ni kuchelewa. Unaweza kuchelewa kwa sababu nyingi. Mosi,
kutokukumbuka muda halisi wa kuanza kwa usaili. Ni rahisi kuchelewa unapokuwa
huna hakika na muda halisi wa kuanza usaili.
Pili, unaweza kuchelewa kwa
sababu huna uhakika na mahali patakapofanyikia usaili. Kubahatisha namna ya
kufika eneo la usaili siku ya usaili, unajiweka kwenye hatari ya kuchelewa na
wakati mwingine hata kushindwa kufika.
Tafuta ramani ya eneo mapema,
jiridhishe na namna utakavyofika. Hivyo itakusaidia sana kukadiria muda wa
kuondoka nyumbani au mahali ulikofikia ili uweze kuwahi usaili.
Ikiwa unahitaji kusafiri umbali
mrefu, usisubiri siku ya mwisho kuanza safari. Fika mapema kwenye eneo lililo
karibu na mahali patakapofanyikia usaili ili upate muda wa kupumzika na kutulia
kifikra.
5.Maandalizi ya mwisho
Unahitaji kuonekana nadhifu siku
ya usaili. Ingawa hulazimiki kuvaa mavazi ya gharama na ya namna fulani, hata
hivyo unahitaji kuandaa nguo za heshima. Epuka kuvaa nguo zitakazotoa picha ya
mtu asiye rasmi. Mavazi mafupi, yanayobana, milegezo, mitindo inayozidi kiasi na
mavazi yenye maandishi hayawezi kuwa chaguo sahihi.
Kadhalika, andaa nyaraka muhimu
kama vyeti halisi, cheti cha kuzaliwa, kitambulisho, barua ya kuitwa kwenye
usaili kama umepewa na nyaraka nyingine kama ulivyoelekezwa. Ingawa nyaraka
hizi zinaweza zisihitajike lakini unapokuwa nazo unakuwa na utulivu wa nafsi na
akili.
AHSANTE.
No comments