NAMNA YA KUJITENGENEZEA MTANDAO WA WATU WANAOKUAMINI
NAMNA YA KUJITENGENEZEA MTANDAO WA
WATU WANAOKUAMINI
Na Mwl. Juma
Rununu: +255762957992
Barua pepe: jumapeter399@gmail.com
Tunaishi kwenye zama ambazo mtu kuwa na kundi kubwa la marafiki kwenye
mitandao ya kijamii inachukuliwa kuwa mafanikio. Mahusiano haya ya mitandaoni
hata hivyo ni nadra kuleta tija kwenye maisha halisi. Ndio kusema, umuhimu umuhimu
wake unabaki kuwa kwenye matangazo ya biashara, kubadilishana taarifa kupitia
arafa, mawasiliano sikizi ama vionwa na shughuli zingine zisizohusisha
mahusiano ya karibu baina ya watu.
Kwa upande mwingine, tunafahamu kuwa mafanikio yetu kibiashara, kazini na
katika maisha kwa ujumla yanategemea kiwango cha ukaribu tunaoujenga na watu na
watu na si idadi ya watu tunaofahamiana nao. Namna gani tunaweza kuaminika na
watu wanaofahamiana nao na hivyo kujenga mtandao wa watu tunaoweza kuwategemea
ni ujuzi tunaouhitaji.
MBINU (05) MUHIMU ZINAZOWEZA KUKUSAIDIA KUJENGA MTANDAO
WA WATU WANAOKUAMINI
Hapa ninakuonesha mbinu tano (05) muhimu zinazoweza kukusaidia kujenga
mtandao imara na watu.
- Lenga kundi mahususi la watu
Unataka kuwa karibu na watu wa kundi gani? Unalenga watu unaoweza kujifunza
kwao, waajiri, wafanyakazi, wenzako, wateja, watu uliowahi kusoma nao, watu
uliowahi kufanya nao kazi au watu wenye taaluma fulani?
Tengeneza orodha ya watu wachache wanaokidhi malengo yako kisha hakikisha
unawasiliana nao mara kwa mara. Unapowatafuta usiishie kusema “nilikuwa nakujulia hali hali tu” bali
nenda mbele kufahamu wanapendelea nini, vitu gani vinawagusa zaidi na shughuli
gani wanaipatia uzito zaidi. Hata hivyo, katika kuwasiliana nao epuka kuonekana
wewe ni mtu usiye na shughuli unayepotezea watu muda.
Pia unaweza kuwa na kundi lingine dogo la watu ambao pengine huwahitaji kwa
saa lakini wanaweza kuwa msaada mkubwa huko uendako. Hawa wanaweza kuwa watu
waliopo kwenye ofisi mbalimbali za umma, jiwekee utaratibu wa kuwasiliana nao
mara kwa mara. Tumia WhatsApp, SMS, mitandao ya kijamii kufanya mawasiliano nao
hata kwa mambo ya kawaida.
- Jifunze kuwasiliana na watu
Watu wengi hatujui nguvu ya mazungumzo tunapokuwa na watu. Hatujui siri ya
kugusa mioyo ya watu tunapozungumza nao. Unaonana na mtu lakini huonekani
kuheshimu muda wa mtu unayezungumza naye.
Mtu anaongea wakati huo huo anahangaika kushika shika simu, haoneshi
uzingativu, hachangamki lakini bado anashangaa inakuwaje watu hawaendelezi
mawasiliano baada ya kuachana naye.
Ikiwa unataka watu wavutiwe na wewe na watamani kuendeleza ukaribu na wewe,
jifunze mbinu za mawasiliano. Unapokutana na mtu, kwa mfano, changamka,
tabasamu, itikia vizuri kile anachokizungumza mtu, ongea kwa ujasiri, uliza
maswali ya maana na pia jibu maswali kwa ufasaha. Unapofanya hivi unaongeza
uwezekano wa kujenga mahusiano ya kudumu.
- Wafanye watu watamani kukufahamu
Mojawapo ya mambo yatakayoongeza uwezekano wa watu kuendeleza ukaribu na
wewe ni uwezo wako wa kuwafanya watu wakudadisi kwa lengo la kukufahamu zaidi.
Usifanye kosa la kumfanya mtu akiachana na wewe awe amechoka na asiwe na shauku
ya kukutana na wewe tena.
Kuongea sana, kujisifu, kulalamika, kuwasema watu ni baadhi ya tabia zinazoweza
kumfanya mtu makini asitamani kukutana na wewe tena. Ukitaka kujenga udadisi
wekeza kwenye maarifa na ujuzi adimu. Jifunze mambo kwa kina kwenye eneo lako
la utaalamu, bobea kwenye kitu na uhakikishe unakijua kwa kina chake.
Unapopata nafasi ya kuzungumza, usifanye kosa la kuonesha unababaisha mambo
kijuu juu. Tumia fursa vizuri kuthibitisha kuwa una kitu cha tofauti ndani yako
na kwamba mtu akiwa karibu na wewe kuna kitu atakifaidi. Huwezi kusahaulika.
- Usisubiri uwe na shida ndipo uwatafute watu
Jifunze kumwagilia mtandao wako hata kabla hujaanza kuuhitaji. Wafanye
unaowafahamu wawe sehemu ya maisha yako na wasikuone kama mzigo. Hakuna mtu
angependa kuwa karibu na mzigo utakaomchelewesha kwenda kule aendako.
Usiwatafute watu pale tu unapokuwa na shida. Usiwe mtu wa kukopa kopa bila
sababu. Kumbuka kila anayekusaidia anapunguza wajibu wake kwako. Utakapomtafuta
siku nyingine wakati wa shida anaweza kukukatalia kwa ujasiri kwa sababu humdai
fadhila.
Jifunze kula na kipofu, wakumbuke watu hata kwenye nyakati ambazo huonekani
kuwa na shida. Kama umeajiriwa wakaribishe watu wako kwenye shughuli zinazohusu
kazi. Ikiwa kuna mikutano inayokaribisha watu kutoka nje ya taasisi tumia fursa
hiyo kuwaita watu wako.
- Tafuta fursa za kuwasaidia watu
Kanuni rahisi kwenye maisha ni kuwasaidia watu kabla hujatarajia wakusaidie
wewe. Jifunze watu wako wa karibu wanahitaji msaada upi na jitahidi usaidie.
Unaposikia mtu unayemfahamu amepatwa na matatizo usisubiri uombwe msaada.
Changamkia matatizo ya watu kwa kutumia uwezo wowote mdogo ulionao.
Unapofanya hivyo unawafanya watu wakuone kama mtu wa msaada anayeweza pia
kutegemewa katika nyakati fulani. Kwa namna hii unavuta watu kwako na haitakuwa
rahisi wapuuze pale utakapohitaji msaada wao.
DONDOO ZA AJIRA NA KAZI
Kwa nini unahitaji mtandao wa ajira (Networking)?
- Mtandao ni sawa na mbegu iliyopandwa ili kesho ama
keshokutwa ikusaidie. Mtandao unaojengwa kwa kuwasaidia wengine unakuwekea
mazingira ya wewe mwenyewe kusaidiwa siku moja.
- Mtandao unaweza kuwa chanzo muhimu cha taarifa
zinazohusu nafasi za kazi. Hata kama una kazi tayari unapofahamiana na
watu wa kada fulani inaweza kuwa rahisi wewe kupata ajira uipendayo.
- Kupitia mahusiano na watu wako wa karibu unaweza
kuwa na watu wanaokuhamasisha kupiga hatua moja mbele. Wakati mwingine
heshima yako inategemea aina ya watu unaoonekana nao.
- Mtandao unakujengea marafiki unaoweza kuwasaidia
pale unapoweza. Unapotoa msaada kwa mtu nafsi yako inapata utoshelevu.
No comments