MAHUSIANO YA KIMAPENZI YASIYO NA TIJA KATIKA MAISHA YA VIJANA WENGI WA KARNE YA 21 WANAOONGOZWA NA TAMAA ZA NGONO
MAHUSIANO YA KIMAPENZI YASIYO NA
TIJA KATIKA MAISHA YA VIJANA WENGI WA KARNE YA 21 WANAOONGOZWA NA TAMAA ZA NGONO.
Na Mwl Juma
Mtunzi wa Makala
Rununu: +255762957992
Moshi-Tanzania
Kipindi cha mwanzo wa ujana kimekuwa ni tatizo kubwa miongoni mwa vijana
wengi wa kidijitali yaani wa kiume na wa kike katika karne ya 21. Hii inatokana
na mabadiliko ya kihisia, kiakili na kimwili yanayoisibu miili ya vijana wengi.
Mabadiliko haya huchochewa kwa kasi na mazingira yanayowazunguka ikiwemo ulaji
wa vyakula chochezi vya ukuaji wa mwili, akili na hisia za miili yao hasa
vyenye protini, fati na madini ya vitamini B complex kwa wingi. Vichochezi hivi
visipozingatiwa vizuri kwa umakini wake kuleta maendeleo chanya katika ukuaji
wa miili ya vijana, husababisha matokeo hasi miongoni mwa vijana ikiwemo
ubakaji, kuanzisha mahusiano ya kingono yasiyo na tija kwa kufuata mihemko ya hisia,
mabadiliko ya kitabia hasa zisizokubalika kwa wanajamii, kupata mimba
zisizotarajiwa ambazo zinasadikiwa ndizo chanzo kikuu cha ongezeko na wimbi
kubwa la watoto wa mitaani na kadhalika.
Wavulana wanapoanza kubalehe na wasichana kuvunja ungo ndiyo mwanzo wa
ujana wao. Kipindi hiki ni cha hatari kwani vijana wengi wa kike na wa kiume
hutaka kujua mambo kwa vitendo na si nadharia pale ambapo hisia za kufanya
ngono zinawaka katika miili yao ikiwa ni pamoja na kupiga punyeto, kujamiana,
kubeba ujauzito, kuanzisha mahusiano hasa ya jinsia tofauti, kutaka kujua namna
ya kuridhishana kingono na jinsi ya kutumia njia za kuepuka kubeba ujauzito
(contraceptives). Kujaribu kufanya jambo pasina uwelewa wa kutosha na mipango ni
hatari.
Chukulia wewe ni dereva unayebeba abiria na ikatokea ukanibeba ndani ya
gari lako kunitoa pointi A kwenda
pointi B, lakini tukiwa barabarani
mara ukaona taa nyekundu za barabarani zimewaka ghafula ukasimamisha gari
nikakuuliza kwanini umesimamisha gari? Ukanijibu kuwa “kwa sababu taa nyekundu za barabarani zimewaka, na huwa ninasimamisha
gari nikiona taa nyekundu zimewaka”. Baadaye simu yako ikaita ukaichukua ukaipokea.
Nikakuuliza kwanini umepokea simu? Ukanijibu kuwa “nimeipokea kwa sababu imeita”. Papo hapo ukaanza kujishangaa
ukijisemea “mimi ni mpumbavu kiasi gani”. Lakini mimi ni mpumbavu kama unavyofikiri? Je,
mara zote unasimama gari unapoona taa nyekundu zimewaka? Na kupokea simu ikiita? Je, hujawahi kuzigonga
taa nyekundu kwa makusudi na ukadai ni bahati mbaya? Je, mara kwa mara hujawahi
kutokupokea simu ulipoisikia ikiita kwa sababu za kudai uko bize unafanya mambo
yako ya msingi?
Hakika siwezi kuilaumu taa nyekundu iliyowaka wala simu iliyoita kwani
hazikufanyi usimame au kupokea simu, ikumbukwe pia hazitusababishi tusimame
wala kupokea simu inayoita. Tunasimama kwa sababu sote tumebeba vitu ndani yetu
shauku yenye uwezo kufanya yote tunayoweza tubaki tukiendelea kupumua katika
uso wa dunia tambala linaloanikwa kila kukicha lakini ndani yake limejaa kiwewe.
Tunapokea simu pindi iitapo kwa sababu wengi wetu pia tuna shauku yenye nguvu
inayotufanya tuongee na yeyote aliye tayari kuongea na sisi.
Hebu fikiri kuhusu uwezekano wa kuigonga taa nyekundu au kuiacha simu iite
wakati huo upo nyumbani peke yako bila kazi yoyote na itakuwa wazi kuwa
kinachokufanya ufanye jambo fulani kipo ndani yako na si nje yako.
Hakuna chochote tunachokifanya kinasababishwa na vinavyotokea nje yetu.
Kama tunaamini kwamba kile tunachokifanya kinasababishwa na nguvu ama
visababishi vilivyo nje yetu hakika tunajifanya kama mashine zilizokufa na si
watu tunaoishi. Kwa sababu tunaishi, tunaweza kuchagua kujibu ama kutokuijibu
simu inayoita bila kujali inatimiza lengo kwa wakati huo.
Vijana wengi wa kiume na wa kike katika karne hii ya 21 wamekuwa na shauku
ya kumiliki wapenzi (girlfriends/boyfriends) kwa sababu ya tamaa zinazowaka
ndani ya miili yao. Hawako tayari kupuuzia kuona taa zinawaka na wao wakiwa
bize wakiendesha magari yao pasipo kusimama na badala yake hubakia wakijitetea kwa
maneno yanayopeperushwa kwa kuelekea katika ombwe lisilo na tija yoyote kuwa eti
wamesimamisha magari kwa sababu taa nyekundu zimewaka.
Baadhi yao hasa vijana wa kiume wanadiliki kununua viwanja kila mahali
wapitapo wasivyovianzishia ujenzi na kuviacha vikiwavutia nyoka na fumo(wanyama
wadogowadogo jamii ya paka wanaochimba mashimo ardhini kama sehemu ya kuishi)
kujianzishia makazi yasiyo rasmi. Vijana hao wamekuwa wakiahidi kuwa viwanja
vyao ipo siku watavianzishia ujenzi lakini cha kushangaza hawana mipango yoyote
madhubuti kutekeleza wanayowaahidi wauzaji wa viwanja.
Watu huwajia wakihitaji viwanja kwa ajili ya kujenga mijengo ya maana
wakiwa na raslimali kedekede ikiwa ni pamoja na matofali, madumu ya rangi
yaliyojazwa hadi pomoni, mifuko ya saruji, vigae (tiles), mabati ya kisasa na
vitu vingine vingi kupendezesha vyumba watakavyovijenga. Lakini cha ajabu
hawapati viwanja na waliovimiliki hawana hata tofali moja la sampuli.
Hivyo, ewe kijana kama unahitaji kuwa na mpenzi jipange uwe na malengo
usiwe ndiyo chanzo kikubwa cha kukatisha ndogo za vijana wa kike ambao tumekuwa
tukiwaahidi tutawaoa na kuboresha maisha yao siku za usoni lakini wakati huo
hatuna mpango wowote wa kuishi nao na kubakia tukiwafanya mithili ya majamvi ya
wageni yanayojaribiwa kama yanakidhi haja wa watumiaji au la. Hii ni hatari
sana kwani matokeo yake ni kuzaa watoto tusiowatarajia katika maisha yetu kwani
uwepo wao wengi wetu tunawachukulia wamezaliwa kwa bahati mbaya na kuwatelekeza
pasipo kuwapatia huduma za msingi ambazo ni haki zao kama binadamu wengine.
Nchini Tanzania, takwimu zinaonesha kuwa karne hii ya 21 kumekuwa na wimbi
kubwa na ongezeko wa watoto wa mitaani ambao haijulikani wazazi wao ni akina
nani. Wengi wao wamezaliwa kama matokeo ya mahusiano yasiyo na tija yaliyolenga
kutibu hisia na mihemko tu bila kujali matokeo yake miongoni mwa vijana wa kike
na wa kiume wanaowaka tamaa katika miili yako na kujiingiza katika ngono zisizo
na malengo chanya kwa maisha ya baadaye.
Ewe mtu wangu wa nguvu, lengo la makala hii ni kutuelimisha sote vijana na
kutusaidia kufanye maamuzi thabiti na malengo yenye tija yatakayowasaidia
watoto wetu ambao ni kizazi kijacho kitakachosimamia maadili na ustawi wa jamii.
Muda utafika tutatoweka sote na watakao baki ni watoto wetu na kama
tumewapandikizia mbegu ya chuki ya kutowalea vizuri ikiwemo kuwatelekeza baada
ya kuwazaa italeta athari hasi kwa kizazi kijacho kinacholimbikiza chuki kwa
wazazi wao wasio na fikra chanya kwa maendeleo yao. Ikumbukwe kuwa tabia ya
mtoto kama ni mbaya inatokana na malezi ya wazazi waliokurupuka kuzaa bila kuwa
na mipango ya kulea watoto wao.
No comments